SERIKALI Mkoani Ruvuma imewafikisha mahakamani wazazi 100 kwa tuhuma za kufanya sherehe baada ya watoto wao kufeli mitihani, FIKRA PEVU imefahamishwa.

Mazingira duni ya kufundishia na kujifunza katika Wilaya ya Tunduru, mkoani huko, yameelezwa ni moja ya sababu inayowafanya wazazi kushawishi watoto wasisome kwa bidii wala kufaulu witihani, ambapo mwanafunzi akifeli mtihani wa darasa la saba hufanyiwa sherehe.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu, ameliambia FIKRAPEVU  Jumatano Aprili 2, mwaka huu, kutokana na hali hiyo serikali ya mkoa imefikisha mahakamani wazazi 100  kwa makosa mbalimbali likiwepo hilo kwa kisingizio cha kukosa karo.

Amesema hali hiyo imetokea katika Wilaya ya Tunduru, huku hali ya Mkoa nayo ikiwa hairidhishi kutokana na mwamko mdogo uliopo kwa wazazi na walezi.

Wanafunzi wanaosoma katika Shule za msingi Wilayani Tunduru mkoani humo, huambiwa na wazazi wao  kuwa wasijaze majibu yaliyo sahihi wanapofanya mitihani, bali wajaze ‘Makorokocho’ ambapo kila anayefeli mtihani huo hufanyiwa sherehe na Wazazi wake.

Hali imeelezwa kuchangia kuifanya Wilaya hiyo kuwa ya mwisho Kimkoa na Kitaifa katika matokeo ya darasa la Saba mwaka jana.

“Tumekuwa tukifanya vizuri katika sekta nyingine lakini sekta ya Elimu kwa kweli ndugu mwandishi tuko nyuma sana pamoja na wazazi, ila tunazidi kuelimisha wazazi wanaozuia watoto kusoma, ikiwa ni pamoja na wale wanaowapa mimba ambao tunashindwa kuwabana wahusika kwamaana mtendewa jambo anashirikiana na mhalifu ili tukose ushahidi Mahakamani,” alisema.

Wakuu wa Idara wawajibike

Mwambungu, amewataka wazazi kuacha tabia hiyo ambapo watakao bainika kufanya hivyo tena watachukuliwa hatua kali za kisheria, ambapo amewaagiza Wakuu wa Idara ya Elimu na Ukaguzi wa shule zote Mkoani humo, kuongeza juhudi za kuongeza kiwango cha ufaulu, kwani Mkoa huo umeshika nafasi ya 151 kati ya Wilaya zote Nchini.

Hata hivyo amesema Vijiji vya Marumba, Nangunguru, Mjala, Mkalekawana, Kidodoma, Mbatamila na Machemba, wazazi au walezi wanaoishi katika Vijiji hivyo wamekuwa chachu ya kudororesha sekta ya elimu na kushindwa kusonga mbele kwa kuwa na mila potovu kwa hawajasoma ambapo amesema Wakuu wa Wilaya husika wamekuwa wakiendesha kampeni ya kuieleza jamii umuhimu wa elimu.

Mitandao ya kijamii

Aidha katika mtandao ikiwemoJamiiforums kumekuwepo na mjadala wa suala hilo, ambapo baadhi ya Wananchi wamelaani kitendo cha mzazi hao, kumfanyia mwanafunzi sherehe akifeli mtihani wa darasa la Saba.

Pamoja na mambo mengine chanzo cha Mkoa huo kutajwa kuwa sekta ya hiyo imedorora, sualala ‘ufinju’ wa bajeti, nalo linatajwa kuchangia sekta hiyo ambayo haikidhi mahitaji, ikiwemo ukaguzi wa Shule na Waalimu kwa ujumla, jambo ambalo Mkuu wa Mkoa amesema ni changamoto ambayo inashughulikiwa na serikali ya Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI).

Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina jumla ya walimu 1047 wanaofundisha Wanafunzi 57,959 (Wavulana 29535 na Wasichana 28424). Ambapo Shule za msingi zilizopo ni 140 huku halmashauri hiyo inakabiliwa na upungufu wa Walimu 402.

- See more at: http://www.fikrapevu.com/wazazi-100-kortini-ruvuma-kusherehekea-watoto-kufeli/#sthash.ANYqnNoo.dpuf

0 comments:

Post a Comment

 
Top
Blogger Template