Stori: IMELDA MTEMA
TIMBWILI la aina yake limetokea nyumbani kwa ‘Beautiful Onyinye’ wa Bongo, Wema Sepetu, kati ya Martin Kadinda na nyota wa filamu za Bongo, Aunt Ezekiel, ‘Kubwa’ lina kisa klizima.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, gogoro zima lilishika nafasi asubuhi ya Aprili 6, 2014 nyumbani kwa Wema, Makumbusho jijini Dar es Salaam, kufuatia Kadinda ambaye ni meneja wa Wema kumvurumishia shutuma Aunt akidai ni mnafiki mkubwa, tena ndiye chanzo cha Kajala Masanja na Wema kutibuana huku akimtaka aondoke.

TWENDE POLEPOLE
Chanzo kilisema, siku hiyo Aunt alilala nyumbani kwa supastaa huyo, lakini asubuhi wakiwa bado wanagalagala kwenye sita kwa sita, Kadinda alifika na kuwakuta hawajaamka, ndipo alipolianzisha.

Kwanza aliwaamsha huku akimshutumu Aunt kwa nini amelala pale wakati ana kwake na ni mke wa mtu?
Mpashaji wetu alizidi kuweka wazi kwamba, baada ya Martin kumuuliza swali hilo, Aunt hakuwa na jibu la moja kwa moja (pengine alikodoa macho tu), ndipo jamaa huyo alipomwanzishia vita ya maneno makali huku akisisitiza aondoke.

KISIKILIZE CHANZO
“Siku hiyo Martin unayemjua wewe hakuwa mwenyewe. Alikuwa mkali sana. Ilifika mahali alimshangaa kwa nini yeye (Aunt) ni mke wa mtu halafu anakwenda kulala nyumbani kwa Wema na si kwake Mwananyamala?

“Alimwambia ujirani wake na Wema ndiyo umekuwa chanzo cha ugomvi wa madam huyo na staa mwenzake wa filamu, Kajala.

“Yeye Martin anaamini kwamba, kuna maneno ambayo Aunt anayasema kwa Wema kuhusu Kajala ndiyo maana sasa hivi hawapikiki. Si unajua kwa sasa, Wema na Aunt ni kama pochi na kwapa?” chanzo kilimwaga mchele na kusisitiza jina lake kufichwa kapuni kama si kibindoni kabisa.

WEMA KATIKATI YA GOGORO
Mtonyo uliendelea kudai kwamba, wakati Martin akizidi ‘kumpelekea’ Aunt na kuifanya nyumba ikikose amani kwa kelele, Wema aliingilia kati na kumhoji meneja wake hivi: “Kama umechukizwa na kitendo cha Aunt kulala hapa, kwa nini unamuingiza Kajala kwenye ugomvi?”

AUNT: WE MARTIN UNA SABABU NYINGINE!
Muda wote huo, Aunt alibaki kimya, lakini madongo yalipozidi alijilipizia kwa kumwambia Martin kwamba, labda ana sababu nyingine lakini siyo kumwingiza katika ugomvi wa Wema na Kajala ambao haujui chanzo chake.

“Aunt alijizuia mwisho akamwambia we Martin una sababu nyingine, kwa nini unaniingiza mimi kwenye ugomvi wa Kajala na Wema?” chanzo kilisema kikimkariri Aunt.

IJUMAA ‘KUBWA’ LAWASAKA WOTE
Baada ya kupata nzitonzito hiyo, paparazi wetu alianza kwa kumtafuta Martin alipopatikana alikiri kutokea kwa ugomvi huo na kusema:

“Nilikuwa najaribu tu kumuelewesha Wema na Aunt kwa kuwa watu kwa hivi sasa wanawatazama kwa mtazamo tofauti kabisa na wanavyoamini wao. Mimi ndiyo nafahamu hivyo.


“Unajua watu wanamsema Aunt vibaya sana, hajui tu. Wanadai kwamba yeye ndiyo chanzo hasa cha ugomvi wa Kajala na Wema, sasa nilivyomkuta amelala pale ndiyo na mimi nikacharuka kwa kuwa kuna mambo ambayo tulikuwa hatujayafanya na Wema kwa sababu Aunt yuko pale,” alisema Martin bila kutaja mambo hayo ni yapi.

WEMA SASA
Kwa upande wake Wema alipopatikana hewani na kuulizwa kuhusu kisanga hicho, naye alikiri kutokea lakini akasema ‘mwisho wa siku’ waliweka mambo sawa.
“Ulikuwa ugomvi wa kawaida, si unajua sisi ni binadamu, Lakini baada ya yote waliweka mambo sawa na shughuli nyingine zikaendelea,” alisema Wema.

Paparazi: Ni kweli yeye ndiyo chanzo cha wewe na Kajala kugombana?
Wema: Noo! Hakuna kitu kama hicho. Kwanza hajui chochote kuhusu mimi na Kajala.

AUNT HOLA!
Juzi, Aunt alitafutwa kwa njia ya simu lakini hakupatikana. Paparazi alifika nyumbani kwake Mwananyamala ambapo wanyeji waliokutwa walisema amesafiri Dubai kwa mume wake.

Paparazi: Naweza kupata namba yake?
Mwenyeji: Aah! Wala hutuna, labda uje siku nyingine.

TUKIRUDI NYUMA
Kwa sasa, Wema na Aunt ni kama ‘mgambo wa jiji na machinga’ kila kukicha wapo sambamba lakini awali, Wema alikuwa na urafiki mkubwa na Kajala.

Wema ndiye aliyemtolea Kajala fedha kiasi cha shilingi milioni 13 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar hivyo kumnusuru na kifungo katika keshi ya mwanadada huyo ya kutakatisha fedha chafu na kuuza nyumba iliyo kwenye dhamana kisheria.

Baada ya kuachiwa huru, Kajala na Wema walikuwa kama ‘bwana afya na bucha la nyama’ huku wengi wakimpongeza Wema kwa uamuzi wake huo mgumu.

Cha ajabu, siku za hivi karibuni, wawili hao wako kama Kaskazini na Kusini kwamba hawawezi kuwa sanjari, kisa kikidaiwa si kimoja. Wengine wanadai chanzo ni Kajala ‘kambeba’ jumla aliyekuwa bwana wa Wema, Clement ‘Kigogo wa Ikulu’.

Wapo pia waliodai kwamba, uadui wao umetokana na Kajala kuanza kuwa tajiri huku Wema akishuka kila kukicha. Lakini Aunt naye amekuwa akitajwatajwa kuchochea uhasama huo.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
Blogger Template