Dar es Salaam. Hatimaye wafanyakazi wa maduka ya Shoprite wameanza kulipwa mafao yao baada ya kupewa barua za kuachishwa kazi na menejimenti.
Walianza kulipwa mafao yao baada ya kuvunjwa kwa mikataba yao ya kazi, malimbikizo ya likizo tangu 2008 na madai mengine.
Mmoja wa viongozi (jina lake tunalihifadhi), aliliambia gazeti hili jana: “Fedha zimeshaingia kwenye akaunti lakini tunajadiliana kama kiasi kilichoingia ndicho, tunawasiliana na Mahakama ya Kazi iliyomwamuru mwajiri atulipe,” alisema.
Alisema jedwali la malipo ya kila mfanyakazi lipo katika Mahakama ya Kazi na jana walikuwa wakifuatilia ili kuhakiki malipo yao.
Kiongozi huyo alisema, licha ya kupewa barua za kuachishwa kazi watatakiwa kufanya kazi mwezi wote wa Aprili kwa makubaliano maalumu na watalipwa mishahara.
Alisema, makubaliano hayo ni kutokana na Shoprite kushindwa kukabidhi maduka kwa Kampuni ya Nakumatt ya Kenya kwa kuwa Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC) bado haijatoa kibali.
Meneja Uhusiano wa FCC, Frank Mdimi alisema, uamuzi wa Nakumatt kukabidhiwa maduka ya Shoprite utajulikana baada ya wakurugenzi na tume hiyo kukutana.
Mdimi alisema wakurugenzi hao hawajakutana kwa sababu wengine wako safarini na wakikutana watatoa uamuzi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment