UTAJIRI wa komediani maarufu nchini Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ ni kufuru! Tena unatisha na sasa anaonekana kuwa miongoni mwa wasanii wanaomiliki fedha na mali nyingi Bongo, Risasi Mchanganyiko linakupa zaidi. Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ akiwa mbele ya usafiri na mjengo wake. HABARI MEZANI Awali, habari kuhusu utajiri wa Masanja ilitua mezani mwa gazeti hili kama kidokezo, hapo mwandishi wetu akaingia mzigoni na kuanza kuchunguza kwa kina mali anazomiliki msanii huyo na kugundua kuwa ni kati ya mastaa mabilionea Bongo. “Masanja sio yule tena. Ana mpunga (fedha) mrefu sana. Hakuna msanii wa maigizo Bongo anayeweza kumfikia kwa sasa. Hao wengine ni mbwembwe tu, lakini pesa imelala kwa Masanja,” kilipasha chanzo chetu. Kikaongeza: “Kwanza ana ghorofa lipo Tabata, hapo ndipo anapoishi. Pia ana magari kibao ya kifahari, mashamba ya mpunga na Kampuni ya OK Security inayolinda sehemu mbalimbali zikiwemo taasisi nyeti nchini. Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ akiwa kwenye pozi na miongoni mwa magari yake. “Ni msanii gani mwenye kampuni kubwa kama ya Masanja? Wengi wanaishia kudai wanatayarisha filamu ambazo hata matunda yake hayaonekani.” Uchunguzi wetu ulibaini ukweli wa mali za msanii huyo na mambo mengine mengi yanayoingia kama vyanzo vya mapato yake. MAGARI SITA Ilibainika kuwa, Masanja anamiliki magari sita, yakiwemo ya kifahari. Baadhi ya magari hayo ni Toyota Land Cruiser V8, Nissan Hardboad na Toyota Verossa. NYUMBA TATU BONGO Pia, mkali huyo wa kuvunja mbavu, anamiliki nyumba tatu za maana jijini Dar es Salaam, moja ni ghorofa ipo Tabata, nyingine Kigamboni na nyingine haifahamiki eneo rasmi ilipo. Hata hivyo, imebainika kuwa mbali na mijengo yake hiyo iliyopo jijini Dar, nyumbani kwao Mbarali, Mbeya ana mjengo wa maana. MASHAMBA KIBAO Msanii huyo hayupo nyuma kwenye kilimo, ana mashamba kadhaa Kigamboni jijini Dar es Salaam lakini linalotia fora ni lile lililopo Mbarali lenye ukubwa wa hekari 50 ambalo analima mpunga. NI MSANII WAMAIGIZO TAJIRI ZAIDI? Kwa utajiri huo, ipo minong’ono kuwa, nyota huyo anaweza kuwa kwenye namba za juu za wasanii wa maigizo wenye mkwanja mrefu. Wengine wanaotajwa kwenye orodha ya waigizaji matajiri Bongo ni Husna Posh ‘Dotnata’, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ na Amri Athumani ‘Mzee Majuto’. MATAJIRI BONGO FLEVA Katika muziki wa Bongo Fleva, wasanii wanaoaminika wana utajiri mkubwa zaidi ni Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, Nasibu Abdul ‘Diamond’ na Joseph Haule ‘Profesa Jay’. Wasanii hao wanamiliki mijengo ya maana, achilia mbali magari ya kifahari na miradi kadhaa. MASWALI KUHUSU MASANJA Utajiri wa Masanja umeonekana kuibuka ghafla huku vyanzo vyake vya kumwingizia kipato vikijulikana ni sanaa ya uigizaji, muziki na huduma ya uchungaji. Je, kwa uigizaji tu katika Kundi la Orijino Komedi ‘OK’ ndiko alikopata mkwanja huo na kuanzisha miradi hiyo mikubwa? Kama ndiyo, kwa nini memba wenzake ndani ya kundi hilo hawana maendeleo makubwa kama yeye? Kazi nyingine ya Masanja ni muziki wa Injili ambapo kwa sasa albamu yake ya Hakuna Jipya iko sokoni. Je, albamu hiyo na shoo anazofanya zinaweza kuwa chanzo cha utajiri huo? Lakini pia Masanja ni mchungaji ambaye anahudumu katika Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) ‘Mito ya Baraka’ lilicho chini ya Askofu Bruno Mwakiborwa. Je, mshahara anaoupata kutokana na huduma hiyo unaweza kuwa chanzo cha mapato yake? Risasi Mchanganyiko halikutaka kupasua kichwa, juzi lilimsaka Masanja kwa simu na kumhoji juu ya mali zake ambapo kwanza alithibitisha kweli anamiliki mali hizo na nyingine ambazo hakupenda kuzitaja. “Ni kweli nina nyumba tatu hapa mjini, kampuni ya ulinzi na mashamba ya mpunga eka 50 nyumbani Mbarali, Mbeya. Kuhusu magari pia ni kweli kabisa. Mimi ni mtumishi sitakiwi kusema uongo,” alisema Masanja

0 comments:

Post a Comment

 
Top
Blogger Template