Twiga Stars imepoteza mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania tiketi ya

kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) baada ya leo kufungwa mabao

2-1 na Zambia (Shepolopolo) kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.



Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika katika mechi hiyo iliyochezeshwa na

mwamuzi Salma Mukansanga timu hizo zilikuwa suluhu.



Wenyeji ndiyo walianza kupata bao lililofungwa na Hellen Mubanga dakika ya

75. Mfungaji huyo aliyeingia kipindi cha pili nchini alimalizia wavuni

mpira uliotemwa na kipa Fatuma Omari.



Dakika nne baadaye Zambia ambao walikuwa wakishangiliwa kwa nguvu na

washabiki wao baada ya kufunga la kwanza, walipata bao la pili ambalo

nahodha wa Twiga Stars, Sophia Mwasikili alijifunga mwenyewe.



Mwasikili alikuwa akijaribu kutoa nje mpira uliopigwa na nahodha wa

Shepolopolo, Mupopo Kabange ambapo ulipishana na kipa Fatuma Omari kabla ya

kujaa wavuni.



Bao la Twiga Stars lilifungwa na Donisia Daniel dakika ya 90. Beki huyo wa

kushoto ambaye pia ni mchezaji wa Tanzanite alipanda mbele kuongeza

mashambulizi ambapo akiwa nje ya eneo la hatari alipiga shuti lililomshinda

kipa Hazel Nali.



Akizungumza baada ya mechi, Kocha wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage alisema

amebaini upungufu katika kikosi chake ambao ataufanyia kazi kabla ya mechi

ya marudiano ili timu yake iweze kusonga mbele.



"Kwa matokeo haya bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi ya

marudiano nyumbani na kusonga mbele," alisema Kaijage.



Twiga Stars iliwakilishwa na Fatuma Omari, Fatuma Bashiru, Donisia Daniel,

Fatuma Issa, Evelyn Sekikubo, Sophia Mwasikili, Vumilia Maarifa, Mwapewa

Mtumwa/Amina Ali, Asha Rashid, Etoe Mlenzi/Zena Khamis na Shelida Boniface.



Timu hiyo inarejea nyumbani kesho kwa ndege ya Fastjet ambapo itatua kwenye

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 7 kamili mchana.
*Boniface Wambura Mgoyo*

*Ofisa Habari na Mawasiliano*

*Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)*

0 comments:

Post a Comment

 
Top
Blogger Template